Remarks
Hillary Rodham Clinton
Secretary of State
Marrakech, Morocco
November 3, 2009


Hotuba ya Waziri wa Mambo ya Nje Hillary Rodhman Clinton
Kwenye Jopo la hali ya Siku Zijazo

Novemba 3, 2009
Marrakech, Morocco


WAZIRI CLINTON: Kwa hiyo ni furaha kubwa kuungana kwenye mjadala huu, na hasa natambua umuhimu wa kuwa na mtawala—mawaziri wa serikali na viongozi wa kijamii wa kiraia wakizungumza pamoja juu ya masuala haya yanayotuhusu sote. Hilo linawezekana kuwa jambo la nadra, lakini halipaswi kuwa hivyo, kwa sababu lengo letu ni kusikiliza, kujifunza na kubuni njia mpya ambazo tunaweza kufanya kazi kama washirika kwa manufaa ya watu tunaowawakilisha.

Kama ninyi wote, nimejionea mwenyewe ukarimu na uwazi wa watu wa Morocco. Na jana, nilipata fursa ya kukutana na Mfalme Mohammed V1 ( wa sita) kuonyesha kufurahishwa kwangu na maendeleo ambayo yamefanyika Morocco; hasa, mageuzi ambayo yametoa uhuru mpya kwa wanawake ambao sasa wanatumia vipaji vyao kuimarisha asasi za kidemokrasia, kuchochea ukuaji wa uchumi, na kupanua kazi za jamii za kiraia.

Katika ziara yangu ya awali katika nchi hii inayovutia miaka 10 iliyopita, nilikuwa na fursa ya kukutana na raia wengi wa Morocco. Nakumbuka vyema kupata nafasi ya kumsikiliza baba mzazi ambaye hakujua kusoma na kuandika, aliyeunga mkono ndoto ya binti yake kuwa daktari na kukutana na waumini wa kike ambao walikuwa wamepiga hatua na kuwa watetezi wa haki za binadamu katika mabaraza ya miji. Mifano kama hii inatukumbusha sisi kwamba kuna mengi ya uzoefu wa Morocco ambayo tunaweza kuyatumia kama mwongozo wa juhudi zetu hivi leo.

Miezi mitano iliyopita mjini Cairo, rais Obama aliitisha mwanzo mpya baina ya Marekani na jumuiya za Kiislamu kote duniani—uhusiano ambao ni mkamilifu badala ya kumulika tu masuala machache ya kisiasa na ulinzi, uhusiano ambao misingi yake ni ushirikiano baina ya watu na vile vile serikali, na uhusiano ambao utadumu kwa muda mrefu. Hayo yalikuwa ni baadhi ya maneno muhimu ambayo aliyatamka rais Obama mjini Cairo, na hotuba yake ilizua hisia nyingi za kuvutiwa duniani kote. Watu wengi walisikia mwito wake na kujiuliza, tunaweza kufanya nini; na wewe Marekani, unaweza kufanya nini; mtazamo wa rais Obama utakuwa na mwelekeo gani katika sera za Marekani; na mwelekeo huo unaweza kutafsiriwaje katika mabadiliko ya maana katika maisha ya kila siku ya watu?

Kama anavyoamini rais Obama na mimi pia, ni matokeo, si maneno, ambayo hatimaye yatakuwa na maana. Uwezeshaji wa kiuchumi, elimu, huduma za afya, na uwezo wa kupata nishati na mikopo, hivi ni vitu vya msingi ambavyo jumuiya zote zinavihitaji ili kustawi. Na Marekani inataka kufuatilia malengo haya ya pamoja kupitia hatua thabiti. Tunajua kwamba maendeleo halisi hutokana na jumuiya zenyewe na hayawezi kulazimishwa kutoka nje, na tunajua kwamba mabadiliko hayatokei siku moja. Kwa hiyo hatutaelekeza juhudi zetu katika miradi ya wakati mmoja, lakini tutajitahidi kushirikiana nanyi nyote katika serikali na jamii za kiraia kujaribu kujenga uwezo wa watu na kuyawezesha mashirika na watu wa eneo kuunda mabadiliko endelevu.

Nimeuagiza Ubalozi wetu kushirikiana na makundi ya kijamii kupata maoni yao jinsi Marekani inavyoweza kuwa mshirika mzuri. Pia nimemteua Mwakilishi Maalum wa Kwanza kabisa wa Marekani kwa jamii za Waislamu. Mawazo tuliyoyasikia yametusaidia kuunda mpango wetu. Farah Pandhith, Mwakilishi wetu Maalum mpya, amesafiri sana na kusikiliza na kurudi na kutoa maoni aliyoyasikia kutoka kwa wale wanaoishi na kufanya kazi za kuboresha maisha.

Sasa, tunamulika medani tatu pana ambazo tunaamini msaada wa Marekani unaweza kuwa na ufanisi. Ya kwanza inatokana na kazi na utafiti uliofanyika kwa miaka mingi. Unapowauliza watu katika nchi zote za eneo hili au popote pale duniani ni jambo gani linalokupa usumbufu mkubwa na ni kitu gani ambacho ungependa kuona kinafanyika tofauti katika siku za mbele, jibu kwa kauli moja ni "Nataka kazi nzuri. Nataka kuongeza kipato. Nataka kuipa familia yangu, hasa watoto wangu, nafasi zaidi." Jibu hili linatolewa katika kila jamii bila kujali mahali ilipo jamii hiyo.

Mara nyingi ninasema kwamba ingawa kipawa ni kitu kilichoenea, fursa si hivyo. Na kwa hiyo tuna nia ya dhati kujenga ngazi za fursa kusaidia kukuza vipaji vingi vilivyomo ndani ya watu wa eneo hili. Mapema mwaka ujao, Rais atakuwa mwandalizi wa Mkutano mkuu wa Ujasiriamali mjini Washington utakaowakusanya watu wanaojishughulisha kuunda biashara ndogo ndogo, kupanua biashara zao, na kuchukua vipaji walivyo navyo na kuvigeuza kuwa chanzo cha mapato kusaidia familia zao.

Tumezindua tovuti kwa ajili ya mkutano huu. Ni www.enterpreneurship.gov/summit Na ninawakaribisha kutoa majina ya wajumbe ambao wanaweza kunufaika kwa kuhudhuria mkutano huu, na tafadhali toa maoni yako juu ya masuala kwenye ajenda. Kwa sababu mkutano huu ni sehemu ya juhudi kabambe za kupanua uungaji wetu wa ujasiriamali katika eneo hili, ikiwa pamoja na kuanzisha vituo vipya vya maendeleo ya biashara. Pia ni matumaini yangu kwamba kwa pamoja, tunaweza kuanzisha mfumo wa kuwashirikisha wajasiriamali ambao utaunganisha aina mbalimbali ya watu wanaoshiriki katika shughuli hizi katika eneo hili na kwingineko.

Kuna mawazo mengi mazuri ambayo hufa kwa sababu hali si muafaka kuyafikisha mawazo hayo sokoni. Kuna watu wengi ambao hufanya kazi kwa bidii kila siku kiasi kwamba hawawezi kutambua manufaa ya kazi hizo kwa kiasi ambacho wanastahili. Sasa tumetoa, kama mjuavyo, mabilioni ya dola katika misaada ya mipango inayoendelea ya moja kwa moja katika eneo hili, kuanzia mpango wa kipato cha jamii katika Yemen hadi mpango wa kuajiriwa vijana huko Jordan hadi kazi tunazozifanya hapa Morocco.

Tumewekeza $700 millioni nchini Morocco kupitia mpango wa Millennium Challenge Corporation Compact. Na huu ni mwelekeo tunaoushughulikia ambao unapanuka na una ushirikiano baina ya serikali yetu na serikali ya watu katika nchi—na kwa mfano huu, Morocco—ambako tunasema hatuko hapa kuwaambia ni kitu gani mnachohitaji kutoka kwetu; tuko hapa kuwauliza ni kitu gani tunachoweza kufanya kuwasaidia kufikia malengo yenu. Katika suala hili, tunasaidia sekta mbili za kilimo—mashamba ya miti ya matunda na uvuvi wa samaki wa kiasi kidogo—na vile vile uhunzi wa vifaa vya mikono na kuimarisha huduma za kifedha na ujasiriamali. Mara nyingi tumesikia kutoka kwa wafanyi biashara ndogo ndogo na za kadiri ambao hawawezi kupata misaada ya kifedha, hawawezi kupata misaada ya kiutendaji ambayo ingewawezesha kupanua biashara zao. Kwa hiyo kwa ushirikiano na serikali ya Morocco, tunatumai kwamba tutasaidia kuwezesha kustawi kwa shughuli zaidi za kiuchumi katika kiwango cha chini, ambacho hatimaye, kuanzia chini, zitajenga ustawi.

Medani yetu ya pili itakuwa ni kuendeleza sayansi na teknolojia, kitu ambacho tumesikia kutoka kwa wengi wenu, kusaidia kutengeneza ajira na kukabiliana na changamoto za utandawazi. Si kitu ambacho hamkijui; ni historia yenu. Lakini ilikuwa ni dunia ya Kiislamu ambayo iliongoza katika sayansi na dawa. Ilikuwa dunia ya Kiislamu ambayo ilifungua mlango kwa kiwango kikubwa cha teknolojia na sayansi ambayo leo tunaichukulia kama kitu cha kawaida. Na sasa tunakabiliwa na changamoto ya utandawazi.
Tutashughulikiaje masuala ya maji? Tutafumbuaje mgogoro wa hali ya hewa? Tutatokomezaje maradhi? Kwa kweli, tunataka kusikiliza jumuiya zenu na tunataka kusaidia jumuiya za Waislamu walio wengi kukuza uwezo wa kukabiliana na changamoto za kiuchumi, kijamii na kimazingira kupitia sayansi, teknolojia na ubunifu.

Wizara ya Mambo ya Nje imeanzisha mpango wa wajumbe wa sayansi. Na ninafuraha kutangaza leo kwamba wajumbe wa kwanza watakuwa wanasayansi watatu mashuhuri wa Kimarekani: Dk. Bruce Albert*, rais wa zamani wa National Academy of Sciences ya Marekani; Dk.Elias Zerhouni, mkurugenzi wa zamani wa National Institutes of Health; na Dk. Ahmad Zawawi, mkemia aliyetuzwa tuzo ya Nobel. Kila mmoja wa watu hawa wamekubali kusafiri hadi Afrika Kaskazini, Mashariki ya Kati, Asia ya Kusini na Kusini Mashariki, kutimiza mamlaka ya rais Obama ya kukuza ushirikiano wa kisayansi na teknolojia. Wizara ya Mambo ya Nje pia itapanua nafasi za maafisa wa mazingira, sayansi, teknolojia, na afya* katika ofisi zetu za ubalozi. Na kugharimia ufumbuzi huu, shirika la kibinafsi la uwekezaji katika nchi za nje, United States Overseas Private Investment Corporation, lijulikanalo kama OPIC linaanzisha mfuko wa teknolojia na ubunifu.

Medani yetu ya tatu ya ushirikiano ni elimu. Wiki iliyopita, nilitangaza uungaji wetu mkono wa mpango wa elimu ya juu nchini Pakistan. Tumeanza pia mpango wa kusaidia ushirikiano baina ya vyuo vikuu vya jumuiya za Marekani na taasisi katika jumuiya za Kiislamu kushirikiana katika ujuzi na kutoa mafunzo kwa wanafunzi kwa lengo la kupata ajira nzuri. Tunapanua nafasi zetu za kusomesha wanafunzi, hasa wanafunzi wa elimu ya sekondari ambao hawajahudumiwa ipasavyo. Mojawapo ya mipango yetu ya ufanisi katika elimu unaitwa Access. Hutoa mafunzo ya lugha ya Kiingereza kwa wanafunzi wenye akili katika jumuiya fukara. Nimejitoa binafsi kuunga mkono mpango huu, na natafuta njia za kutoa msaada zaidi, kwa sababu nimejionea mwenyewe nguvu zake.

Mapema mwaka huu, nilitembelea darasa la Access mjini Ramallah. Niliingia katika mjadala wa kuvutia wa Mwezi wa Historia ya Wanawake. Hawa ni wanafunzi ambao hawakutoka kwenye familia za kisomo, lakini walikuwa ni wanafunzi wenye tamaa ya kujiendeleza na hamasa kama ile tuliyosikia ikielezewa na mwenzetu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina, kuhusu mwanawe. Tunataka kuunda fursa zaidi kwa wanafunzi kama hawa ili waweze kutimiza uwezo wao waliopewa na Mwenyezi Mungu.

Na hili linatuelekeza kwenye kipaumbele inayohusiana—kuwawezesha wanawake. Nimesema kama baadhi yenu mjuavyo, kwa miaka mingi, na rais Obama alilisema Cairo, hakuna nchi inayoweza kufikia maendeleo halisi au kufikia uwezo wake pale nusu ya raia wake wanapoachwa nyuma. Wasichana wadogo wanaponyimwa nafasi za elimu, hatujui tunachokipoteza kwa sababu hawataweza kuchangia ustawi na maendeleo ya nchi zao.

Marekani imemteua balozi wetu wa kwanza Mwakilishi katika Masuala ya Wanawake duniani, Balozi Melanne Verveer. Tunaunga mkono kwa dhati mwito uliotolewa katika Jopo la mwaka jana kuhusu Hali ya siku zijazo ya kuundwa kwa taasisi ya eneo inayoshughulikia masuala ya jinsia kusaidia kuendeleza uwezeshaji wa wanawake katika kila fani, kisiasa, kiuchumi, kielimu, kisheria, kijamii na kiutamaduni. Na tuna shauku ya kushirikiana na serikali nyingine na jumuiya za kiraia kuanzisha mpango huu karibuni. Na tutatoa fedha za kwanza za kugharimia kuufanya uwe na kipaumbele.

Tunataka kusaidia juhudi za jumuiya za kiraia duniani kote kwa sababu tunaamini kwamba jumuiya za kiraia zinasaidia kuzifanya jumuiya kuwa imara zenye ustawi. Zinasaidia kusukuma ustawi wa kiuchumi ambao hunufaisha idadi kubwa ya watu. Na zinatoa msukumo kwa asasi za kisiasa kuwa macho na kuwajibika kwa watu inaowahudumia. Kwa hiyo Marekani inaanzisha hatua inayoitwa Civil Society 2.0 Juhudi hizi zilizopangwa zitatoa teknolojia mpya kwa mashirika ya jumuiya za kiraia. Tutatuma wataalamu katika teknolojia ya digital na mawasiliano kusaidia kujenga uwezo.

Sasa, hizi ni baadhi ya njia ambazo Marekani inafuatilia mtazamo wa rais Obama kuhusu uhusiano mpya. Kazi yetu inatokana na kuwawezesha watu binafsi badala ya kueneza itikadi; kusikiliza na kuzingatia mawazo ya wengine badala ya kulazimisha maoni yetu; na kujenga ushirikiano endelevu na ulio mpana. Tunaamini kwamba licha ya tofauti zetu, kuna mengi yanayotuweka pamoja. Akina baba na mama duniani kote wanataka usalama na fursa kwa mabinti na watoto wao wa kiume. Watu kila mahali wanataka kuwa na jukumu katika maamuzi yanayowahusu, kutaja mahitaji yao mbele ya viongozi wao wasikike, na kusaidia kubuni hali yao ya siku zijazo.

Pia nataja kubainisha kwamba Marekani inaunga mkono kuwepo amani kamili katika Mashariki ya Kati. Najua hili ni suala lenye uzito mkubwa na mvuto miongoni mwa nchi zilizowakilishwa hapa, lakini hata nje ya eneo hili. Tumejitoa kuunga mkono ufumbuzi wa nchi mbili, na tumepania na tunakazana kulisaka lengo hilo. Ni muhimu kwamba sote pamoja tushughulikie lengo hilo. Na nafikiri kuwa inahitaji pande zote ziwe waangalifu juu ya tunachosema, aina ya matokeo yake ambayo yanaeleweka, lakini tunahitaji kufanya kazi pamoja katika moyo wa kupania kuelekea lengo la pamoja la kupatikana kwa amani kamaili.

Ninaamini kwa dhati kwamba inaweza kupatikana. Naamini kwamba kujitoa kwa rais Obama kunaeleweka. Na ninaamini kwamba kwa msaada wenu, tunaweza kupata njia kupitia historia ngumu na iliyopindika ambayo mara nyingi inatuzuia kufanya maendeleo katika suala hili muhimu. Kama viongozi wa nchi ambazo zina maslahi ya moja kwa moja na zinajali sana masuala yote ya hatima ambayo lazima yafumbuliwe, ningewaomba kufikiria jinsi tunavyoweza kuonyesha kujitoa kwetu ambako kunahitajika kwetu kuweza kusonga mbele.

Sasa, tunaweza kudumisha utiifu wetu kwa yaliyopita, lakini hatuwezi kubadilisha yaliyopita. Hata tukisema kiasi gani juu yake, yamekwishapita. Au tunaweza kushirikiana pamoja kufuata mtazamo na uhamasishaji wa rais Obama katika kusaidia kuunda hali ya siku za mbele ambayo itakuwa bora zaidi kwa watoto wote wa Wapalestina na familia za Wayahudi. Nina matumaini kwamba tunaweza kufanikiwa katika kuunda ulimwengu bora kwa pamoja, kwa sababu ninajua kinachotusubiri huko mbele kama tutafanya hivyo.

Na nawashukuru kwa kutayarisha jopo kuhusu hali ya siku za mbele, kwa sababu hicho ni kitu ambacho inatubidi kuamua pamoja. Na nashukuru kwa nafasi ya kuwa hapa kuendeleza mtazamo wa hotuba ya rais mjini Cairo, lakini kwenda kwenye hatua thabiti na matokeo dhahiri ambayo ni ya lazima, kama ni kupatikana amani, kuunda ajira, au kuelimisha watoto wetu ili watu tunaowawakilisha waweze kuona maisha yao yakiwa bora zaidi, kwani hatimaye, hicho ndicho sote tumejitoa kukifanikisha. Asanteni sana.